Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 12

12
Waisraeli wamwasi Rehoboamu
(2 Nyakati 10:1-19)
1Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme. 2Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri. 3Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, 4“Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
5Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
6Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?”
7Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
8Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia. 9Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?”
10Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi.’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”
12Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” 13Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri alilopewa na wazee, 14akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.” 15Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kutimiza neno ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni.
16Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:
“Je, tuna fungu gani kwa Daudi?
Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese?
Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli!
Angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”
Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. 17Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
18Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita na kutorokea Yerusalemu. 19Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.
20Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.
21Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, vijana wenye uwezo elfu mia moja na themanini, ili kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
22Lakini neno la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu: 23“Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na nyumba yote ya Yuda na Benyamini, na watu wengine wote, 24‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Mwenyezi Mungu na kurudi nyumbani, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameagiza.
Ndama za dhahabu huko Betheli na Dani
25Kisha Yeroboamu akaimarisha Shekemu, na kuuzungushia ngome katika nchi ya vilima ya Efraimu, na akaishi huko. Kutoka huko, akaenda akajenga Penueli#12:25 au Penieli.
26Yeroboamu akawaza moyoni mwake, “Kuna uwezekano wa ufalme kurudia nyumba ya Daudi. 27Kama watu hawa watapanda kwenda kutoa dhabihu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu, mioyo yao itamrudia bwana wao, Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua mimi na kurudi kwa Mfalme Rehoboamu.”
28Baada ya kutafuta ushauri, mfalme akatengeneza ndama wawili wa dhahabu. Akawaambia watu, “Ni gharama kubwa kwenu kukwea kwenda Yerusalemu. Hii hapa miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.” 29Ndama mmoja akamweka Betheli, na mwingine akamweka Dani. 30Nalo jambo hili likawa dhambi, watu wakawa wanaenda hadi Dani kumwabudu huyo aliyewekwa huko.
31Yeroboamu akajenga nyumba za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia, na kuwateua makuhani kutoka watu wa aina zote, ijapokuwa hawakuwa Walawi. 32Pia Yeroboamu akaanzisha sikukuu katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, kama sikukuu iliyokuwa ikifanyika huko Yuda, na akatoa dhabihu juu ya madhabahu. Haya aliyafanya huko Betheli, akitoa dhabihu kwa ndama alizotengeneza. Huko Betheli akawaweka makuhani katika mahali pa juu pa kuabudia miungu aliyotengeneza. 33Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouchagua mwenyewe, alitoa dhabihu juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga huko Betheli. Kwa hiyo akaanzisha sikukuu kwa ajili ya Waisraeli, na akapanda madhabahuni kutoa sadaka.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 12: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia