Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11

11
Wakeze Sulemani
1Mbali na binti Farao, Mfalme Sulemani aliwapenda wanawake wengi wa kigeni: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. 2Walitoka katika mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Sulemani akakaza kuwapenda. 3Alikuwa na wake mia saba, binti za uzao wa kifalme, na masuria mia tatu; nao wake zake wakampotosha. 4Kadiri Sulemani alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitoa kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake. 5Sulemani akafuata Ashtorethi, mungu wa kike wa Wasidoni, na Moleki#11:5 Moleki au Milkomu ni mungu aliyekuwa akiabudiwa na Waamoni; alikuwa chukizo kwa sababu watoto walitolewa kafara kwake. mungu wa Waamoni, aliyekuwa chukizo. 6Kwa hiyo Sulemani akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu; hakumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake.
7Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Sulemani alijenga mahali pa juu pa kuabudia Kemoshi mungu wa Wamoabu, aliyekuwa chukizo, na pa kuabudia Moleki mungu wa Waamoni, aliyekuwa chukizo. 8Akafanya vivyo hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.
9Mwenyezi Mungu akamkasirikia Sulemani kwa sababu moyo wake uligeuka mbali na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekuwa amemtokea mara mbili. 10Ingawa alikuwa amemkataza Sulemani kufuata miungu mingine, Sulemani hakutii amri ya Mwenyezi Mungu. 11Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa huu ndio msimamo wako, na hukushika agano langu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitakunyang’anya ufalme na kumpa mmoja wa walio chini yako. 12Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi baba yako, sitafanya jambo hili wakati wa uhai wako. Nitaurarua kutoka mikononi mwa mwanao. 13Lakini pia sitaurarua ufalme wote kutoka kwake, bali nitampa kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu na kwa ajili ya Yerusalemu, ambao nimeuchagua.”
Adui za Sulemani
14Kisha Mwenyezi Mungu akamwinua adui dhidi ya Sulemani, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa ufalme wa Edomu. 15Hapo awali Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa ameenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote katika Edomu. 16Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, hadi walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu. 17Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Edomu waliokuwa wamemhudumia baba yake. 18Wakatoka Midiani wakaenda hadi Parani. Wakawachukua watu kutoka Parani, wakaenda nao Misri kwa Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba na shamba, na pia chakula.
19Farao akapendezwa sana na Hadadi, hata akampa dada ya mkewe, Malkia Tapenesi, awe mke wake. 20Huyo dada yake Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko, Genubathi akaishi pamoja na watoto wa Farao.
21Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amelala na baba zake, na kwamba Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi pia amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili nirudi nchi yangu.”
22Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?”
Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!”
23Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Sulemani, Rezoni mwana wa Eliada, aliyekuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba. 24Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walienda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki. 25Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Sulemani, kuongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramu#11:25 yaani Shamu na akawa mkatili kwa Israeli.
Yeroboamu anaasi dhidi ya Sulemani
26Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Sulemani, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua.
27Haya ndio maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Sulemani alikuwa amejenga Milo#11:27 maana yake Boma la Ngome naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake. 28Basi Yeroboamu alikuwa mtu mwenye nguvu na hodari; naye Sulemani alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yusufu.
29Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani, 30naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili. 31Kisha akamwambia Yeroboamu, “Jichukulie vipande kumi, kwa kuwa hivi ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemavyo: ‘Tazama, ninaenda kumnyang’anya Sulemani ufalme na kukupa makabila kumi. 32Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja. 33Nitafanya haya kwa sababu wameniacha na kuabudu Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakuenda katika njia zangu wala kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Sulemani, alivyofanya.
34“ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote mkononi mwa Sulemani; nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu. 35Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi. 36Nitampa mwanawe kabila moja ili Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu. 37Lakini wewe, Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala yale yote moyo wako unayotamani; utakuwa mfalme wa Israeli. 38Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kushika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli. 39Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya haya, lakini siyo milele.’ ”
40Sulemani akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko hadi Sulemani alipofariki.
Kifo cha Sulemani
(2 Nyakati 9:29-31)
41Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionesha, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za Sulemani? 42Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu. 43Kisha Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 11: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia