1 Wafalme 10
10
Malkia wa Sheba amtembelea Sulemani
(2 Nyakati 9:1-12)
1Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani na uhusiano wake na jina la Mwenyezi Mungu, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. 2Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Akaenda kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. 3Sulemani alimjibu maswali yake yote; hapakuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme hata asiweze kumwelezea. 4Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, 5chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipatwa na mshangao mkubwa.
6Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. 7Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. 8Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako! 9Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka kwenye kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Mwenyezi Mungu wa milele kwa Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”
10Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini#10:10 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5. za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezo na vito vya thamani. Kamwe havijawahi kuletwa tena vikolezo vingi kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.
11(Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena zikaleta shehena kubwa ya miti ya msandali, na vito vya thamani kutoka huko. 12Mfalme alitumia miti ya msandali kutengenezea nguzo za Hekalu la Mwenyezi Mungu na za jumba la kifalme, na kutengenezea vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Miti mingi ya msandali kiasi hicho haijawahi kuletwa au kuonekana tangu wakati ule.)
13Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
Fahari ya Sulemani
(2 Nyakati 9:13-28)
14Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta mia sita sitini na sita (666)#10:14 Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25., 15mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Waarabu na watawala wa nchi.
16Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa mia mbili kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli mia sita#10:16 Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5.. 17Akatengeneza pia ngao ndogo mia tatu za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu#10:17 Mane 3 za dhahabu ni sawa na kilo 1.7. za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
18Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. 19Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita, na egemeo lenye mviringo juu yake. Kila upande wa kiti ulikuwa na mahali pa kuegemeza mkono, na simba aliyesimama kando kila upande. 20Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kiti kama hicho kiliwahi kutengenezwa katika ufalme mwingine wowote.
21Vyombo vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Sulemani. 22Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara#10:22 au za Tarshishi (taz. 1 Wafalme 22:48; 2 Nyakati 9:21; 20:36; Isaya 2:16; 60:9). baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Mara moja katika kila miaka mitatu zilirudi zikiwa zimebeba dhahabu, fedha na pembe za ndovu, na sokwe na nyani.
23Mfalme Sulemani alikuwa na utajiri mkubwa na mwenye hekima kuliko wafalme wote wa dunia. 24Dunia yote ikatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. 25Kila mwaka, kila mtu aliyekuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezo, farasi na nyumbu.
26Sulemani alikusanya magari ya vita na farasi. Akawa na magari ya vita elfu moja mia nne, na farasi elfu kumi na mbili, ambayo aliyaweka katika miji ya magari ya vita, na mengine akawa nayo huko Yerusalemu. 27Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima. 28Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue#10:28 yaani Kilikia. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue. 29Walinunua magari ya vita kutoka Misri kwa shekeli mia sita za fedha#10:29 Shekeli 600 za fedha ni sawa na kilo 7. kila moja, na kila farasi kwa shekeli mia moja na hamsini#10:29 Shekeli 150 za fedha ni sawa na kilo 1.7.; na wakawauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu#10:29 yaani Washamu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.