Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 14:21-31

1 Wafalme 14:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni. Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao. Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 14:21-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arubaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa BWANA; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani. Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi. Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.

1 Wafalme 14:21-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa BWANA; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani. Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi. Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.

1 Wafalme 14:21-31 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kuwa mfalme, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni. Yuda wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu kuliko baba zao walivyofanya. Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia, mawe ya kuabudiwa, na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda. Kulikuwa na hata mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi. Watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu. Akachukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza. Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama; alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.