1 Wafalme 14:21-31
1 Wafalme 14:21-31 NENO
Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kuwa mfalme, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni. Yuda wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu kuliko baba zao walivyofanya. Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia, mawe ya kuabudiwa, na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda. Kulikuwa na hata mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi. Watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu. Akachukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza. Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama; alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.