Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 14:21-31

1 Fal 14:21-31 SUV

Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa BWANA; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani. Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi. Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.