2 Wakorintho 10:1-11
2 Wakorintho 10:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali niwapo mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo. Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia. Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia. Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu ya Mungu yenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo. Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii. Nyinyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo. Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa – uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa – hata hivyo sijuti hata kidogo. Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha nyinyi kwa barua zangu. Mtu anaweza kusema: “Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu.” Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi.
2 Wakorintho 10:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu; naam, naomba kwamba nikiwapo, nisiwe na ujasiri kwa uthabiti ambao nahesabu kuwa nao juu ya wale wanaodhania ya kuwa sisi tunaenenda kwa jinsi ya mwili. Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia. Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo ndivyo sisi nasi tulivyo. Maana, nijapojisifu zaidi kidogo kwa ajili ya mamlaka yetu, (tuliyopewa na Bwana, tupate kuwajenga wala si kuwaangusha), sitatahayarika; nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu. Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu. Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo.
2 Wakorintho 10:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu; naam, naomba kwamba nikiwapo, nisiwe na ujasiri kwa uthabiti ambao nahesabu kuwa nao juu ya wale wanaodhania ya kuwa sisi tunaenenda kwa jinsi ya mwili. Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia. Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi. Maana, nijapojisifu zaidi kidogo kwa ajili ya mamlaka yetu, (tuliyopewa na Bwana, tupate kuwajenga wala si kuwaangusha), sitatahayarika; nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu. Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu. Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo.
2 Wakorintho 10:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! Nawaomba nitakapokuja kwenu nisipaswe kuwa na ujasiri dhidi ya watu fulani kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata mtazamo wa ulimwengu huu. Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. Tunaangusha mawazo na kila kitu kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi. Tena tunakuwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, hapo kutii kwenu kutakapokamilika. Mnayaangalia yaliyo mbele ya macho yenu tu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. Basi hata nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana Isa alitupatia ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni mdhaifu, na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” Watu kama hao wajue ya kuwa yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.