2 Wakorintho 10
10
Paulo atetea huduma yake
1Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2Nawaomba nitakapokuja kwenu nisipaswe kuwa na ujasiri dhidi ya watu fulani kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata mtazamo wa ulimwengu huu. 3Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. 5Tunaangusha mawazo na kila kitu kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi. 6Tena tunakuwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, hapo kutii kwenu kutakapokamilika.
7Mnayaangalia yaliyo mbele ya macho yenu tu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. 8Basi hata nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana Isa alitupatia ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. 9Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. 10Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni mdhaifu, na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” 11Watu kama hao wajue ya kuwa yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.
12Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonesha ya kuwa hawana busara. 13Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ya huduma ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama ambavyo ingekuwa tusingekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi. 15Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, ndivyo eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.”#10:17 Yeremia 9:24 18Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Mwenyezi Mungu humsifu.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.