2 Wakorintho 11
11
Paulo na mitume wa uongo
1Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2Ninawaonea wivu, wivu wa kiungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Al-Masihi kama mabikira safi. 3Lakini nina hofu kuwa, kama vile Hawa alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Al-Masihi. 4Kwa sababu mtu akija na kuwahubiria Isa mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.
5Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu”. 6Inawezekana mimi si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
7Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8Niliyanyang’anya makundi mengine ya waumini kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nilipopungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walitimiza mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10Kwa hakika kama vile kweli ya Al-Masihi ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
13Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Al-Masihi. 14Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15Kwa hiyo basi si ajabu kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
Paulo ajivunia mateso yake
16Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana Isa angesema, bali kama mjinga. 18Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyang’anya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya. 21Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!
Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo. 22Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Ibrahimu? Mimi pia ni mzao wa Ibrahimu. 23Je, wao ni watumishi wa Al-Masihi? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja. 25Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa; 26nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. 28Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makundi yote ya waumini. 29Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?
30Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu. 31Mungu na Baba#11:31 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. wa Bwana wetu Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. 32Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. 33Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.