2 Wakorintho 11:25-33
2 Wakorintho 11:25-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa. Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo. Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote. Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi. Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu. Mungu na Baba wa Bwana Yesu – jina lake litukuzwe milele – yeye anajua kwamba sisemi uongo. Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili anikamate. Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.
2 Wakorintho 11:25-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mara tatu nilipigwa kwa bakora; mara moja nilipigwa kwa mawe; mara tatu nilivunjikiwa jahazi; kutwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Mbali na mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski mtawala wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikateremshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.
2 Wakorintho 11:25-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake. e.
2 Wakorintho 11:25-33 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa; nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makundi yote ya waumini. Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike? Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu. Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.