2 Samueli 20:1-12
2 Samueli 20:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa ikawa kwamba huko Gilgali kulikuwa na mtu mmoja mlaghai aitwaye Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini. Basi Sheba alipiga tarumbeta, na kusema, “Hatuna fungu lolote kwa Daudi, hatuna sehemu yetu katika huyo mwana wa Yese. Enyi watu wa Israeli, kila mmoja na ajiendee hemani kwake!” Hivyo, watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi, wakamfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda walimfuata mfalme Daudi kwa uaminifu toka mto Yordani mpaka mjini Yerusalemu. Hatimaye, Daudi aliwasili nyumbani kwake mjini Yerusalemu. Mfalme aliwachukua masuria wake kumi ambao alikuwa amewaacha kuangalia nyumba yake, akawaweka kwenye nyumba moja chini ya ulinzi, akawatunza vizuri, lakini hakulala nao. Hivyo, masuria hao wakawa wametiwa ndani hadi siku za kufa kwao, wakaishi kana kwamba, walikuwa wajane. Kisha, mfalme akamwambia Amasa, “Nikusanyie watu wote wa Yuda katika siku tatu, na wewe mwenyewe uwepo.” Basi, Amasa akaenda kuwaita watu wa Yuda. Lakini akachelewa kurudi katika wakati ule aliopangiwa na mfalme. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.” Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini. Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu. Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili. Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri. Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo.
2 Samueli 20:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hadi Yerusalemu. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hadi siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa. Amasa akaenda kuwakusanya watu wa Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kutuponyoka. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akienda, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kulia ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao tumboni, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri. Akasimama karibu naye mmoja wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama.
2 Samueli 20:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hata kufika Yerusalemu. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hata siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa. Amasa akaenda kuwakusanya Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kujiponya machoni petu. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akiendelea, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao wa tumbo, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri. Akasimama karibu naye mmojawapo wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama.
2 Samueli 20:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Hatuna fungu katika Daudi, wala hatuna sehemu katika mwana wa Yese! Kila mtu aende hemani mwake, enyi Israeli!” Kwa hiyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini watu wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani mpaka Yerusalemu. Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kuangalia jumba la kifalme na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane mpaka kifo chao. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite watu wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” Lakini Amasa alipokwenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” Hivyo watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na wapiganaji mashujaa wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri. Wakati walikuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kwenye kiuno wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka kwenye ala. Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri. Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani mpaka kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.