2 Samweli 20:1-12
2 Samweli 20:1-12 NENO
Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Hatuna fungu katika Daudi, wala hatuna sehemu katika mwana wa Yese! Kila mtu aende kwenye hema lake, enyi Israeli!” Kwa hiyo wanaume wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini wanaume wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani hadi Yerusalemu. Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kutunza jumba la kifalme, na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane hadi kifo chao. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” Lakini Amasa alipoenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara kuliko Absalomu. Wachukue watumishi wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” Hivyo watumishi wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na mashujaa wenye nguvu wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri. Walipokuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kiunoni wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka ala. Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri. Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani hadi kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.