2 Samweli 20:1-12
2 Samweli 20:1-12 SRUV
Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hadi Yerusalemu. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hadi siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa. Amasa akaenda kuwakusanya watu wa Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kutuponyoka. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akienda, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kulia ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao tumboni, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri. Akasimama karibu naye mmoja wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama.