2 Samweli 20
20
Sheba aasi dhidi ya Daudi
1Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti,
“Hatuna fungu katika Daudi,
wala hatuna sehemu
katika mwana wa Yese!
Kila mtu aende kwenye hema lake,
enyi Israeli!”
2Kwa hiyo wanaume wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini wanaume wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani hadi Yerusalemu.
3Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kutunza jumba la kifalme, na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane hadi kifo chao.
4Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” 5Lakini Amasa alipoenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
6Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara kuliko Absalomu. Wachukue watumishi wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” 7Hivyo watumishi wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na mashujaa wenye nguvu wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
8Walipokuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kiunoni wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka ala.
9Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. 10Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” 12Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani hadi kwenye shamba na kutupia nguo juu yake. 13Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walikusanyika na kumfuata. 15Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumzingira Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wakijaribu kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini, 16mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.” 17Yoabu alienda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?”
Akamjibu, “Ndiye mimi.”
Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
18Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri. 19Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Mwenyezi Mungu?”
20Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu. 21Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Mkabidhini mtu huyu mmoja kwangu, nami nitajiondoa katika mji huu.”
Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
22Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani mwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
23Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli;
Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;
24Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa;
Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
25Sheva#20:25 au Shausha (1 Nyakati 18:16) alikuwa mwandishi;
Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
26na Ira Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 20: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.