2 Samweli 21
21
Wagibeoni walipiza kisasi
1Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”
2Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa sehemu ya Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.) 3Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa Mwenyezi Mungu?”
4Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.”
Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
5Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kupanga njama dhidi yetu ili tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli, 6tupatieni wazao wake saba wa kiume, tuwaue hadharani mbele za Mwenyezi Mungu huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na Mwenyezi Mungu.”
Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
7Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za Mwenyezi Mungu kati ya Daudi na Yonathani. 8Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi. 9Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za Mwenyezi Mungu. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.
10Rispa binti Aya akachukua gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno hadi mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama mwitu wakati wa usiku. 11Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya, 12alienda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabesh-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.) 13Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.
14Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.
Vita dhidi ya Wafilisti
(1 Nyakati 20:4-8)
15Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana. 16Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai#21:16 yaani majitu., ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli mia tatu za shaba#21:16 Shekeli 300 za shaba ni sawa na kilo 3.5., alikuwa amejifunga upanga mpya, naye akasema atamuua Daudi. 17Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutaenda tena nasi vitani, ili taa ya Israeli isije ikazimwa.”
18Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai.
19Katika vita vingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimuua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.
20Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwa na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita kila mguu: jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai. 21Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.
22Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.