Danieli 10:15-21
Danieli 10:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Alipokuwa ananiambia maneno hayo, niliangalia chini bila kuweza kuongea. Kisha, mmoja mwenye umbo la binadamu, aliigusa midomo yangu, nami nilifungua midomo yangu na kumwambia huyo aliyesimama karibu nami, ‘Ee bwana, maono haya yameniletea maumivu makali hata nimeishiwa nguvu. Mimi ni kama mtumwa mbele ya bwana wake. Nawezaje kuzungumza nawe? Sina nguvu na pumzi imeniishia!’ “Yule mmoja aliyeonekana kama mwanaadamu akanigusa kwa mara nyingine, akanitia nguvu. Akaniambia, ‘Usiogope wewe unayependwa sana, uko salama. Uwe imara na hodari.’ Aliposema nami, nilipata nguvu, nikamwambia, ‘Bwana, umekwisha niimarisha; sema kile ulichotaka kusema.’ Naye akaniambia, ‘Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa ni lazima nirudi kupigana na malaika mlinzi wa Persia. Halafu, nitakapokuwa nimemshinda, malaika mlinzi wa mfalme wa Ugiriki atatokea. Lakini nitakujulisha yale yaliyoandikwa katika kitabu cha ukweli. Sina mwingine wa kunisaidia kuwashinda hawa isipokuwa Mikaeli, malaika mlinzi wenu.
Danieli 10:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu. Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikubakia na nguvu. Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu. Kisha mmoja mfano wa mwanadamu akanigusa tena, akanitia nguvu. Akasema, Ee mtu upendwaye sana, usiogope; amani na iwe kwako, uwe na nguvu, naam, uwe na nguvu. Aliposema nami nikapata nguvu, nikasema, Ee Bwana wangu, na aseme Bwana wangu; kwa maana umenitia nguvu. Ndipo akasema, Je! Unajua sababu iliyonileta kwako? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Ugiriki atakuja. Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.
Danieli 10:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu. Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikusaziwa nguvu. Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu. Kisha mmoja mfano wa mwanadamu akanigusa tena, akanitia nguvu. Akasema, Ee mtu upendwaye sana, usiogope; amani na iwe kwako, uwe na nguvu, naam, uwe na nguvu. Aliposema nami nikapata nguvu, nikasema, Ee Bwana wangu, na aseme Bwana wangu; kwa maana umenitia nguvu. Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja. Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.
Danieli 10:15-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Alipokuwa akiniambia haya, nilisujudu, uso wangu ukigusa chini, nikawa bubu. Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nami nimeishiwa nguvu. Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia, hata ninashindwa kupumua.” Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.” Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.” Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja. Lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.