Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9:1-19

Danieli 9:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

“Katika mwaka Dario mwana wa Ahasuero, Mmedi, alipoanza kutawala juu ya milki ya Wakaldayo, mimi Danieli nilikuwa nikivisoma kwa makini vitabu vitakatifu, na humo nikaelewa maana ya jambo lile Mwenyezi-Mungu alilomfahamisha nabii Yeremia kuhusu ile miaka sabini, muda ambao utahusika na kuharibiwa kwa Yerusalemu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema: “Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako. Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako waliongea na wafalme wetu, wakuu wetu, wazee wetu na taifa letu lote. Kwako, ee Bwana, kuna uadilifu, lakini sisi daima tumejaa aibu. Jambo hili ni kweli kwetu sote tuishio Yudea, wakazi wa mji wa Yerusalemu na Waisraeli wote ambao umewatawanya katika nchi za mbali na za karibu kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea. Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi. Tulikataa kukusikiliza, ee Bwana, Mungu wetu; hatukuishi kulingana na sheria zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii. Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako. Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani. Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako. Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza. “Na sasa ee Bwana, Mungu wetu, uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa nguvu yako kuu na kulifanya jina lako litukuke mpaka sasa, tunasema kwamba tumetenda dhambi; tumefanya maovu. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki usiukasirikie wala kuughadhibikia mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Watu wote wa nchi za jirani wanaudharau mji wa Yerusalemu na watu wako, kwa sababu ya dhambi zetu na maovu waliyotenda wazee wetu. Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa. Tega sikio, ee Mungu wangu; angalia uone taabu tulizo nazo na jinsi unavyotaabika huo mji uitwao kwa jina lako. Tunakutolea maombi yetu si kwa sababu tumetenda haki, bali kwa sababu wewe una huruma nyingi. Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako!

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nilifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kusihi kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna aibu, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna aibu, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameivunja sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na kiapo kile kilioandikwa katika Sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi BWANA anayachungulia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi BWANA ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-19 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala wa ufalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini. Kwa hiyo nikamgeukia Mwenyezi Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa gunia na kujipaka majivu. Nikamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake, tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi. “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: watu wa Yuda, na wakaaji wa Yerusalemu, na Waisraeli wote, walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu tulikosa uaminifu kwako. Ee Mwenyezi Mungu, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake. Hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuzishika sheria alizotupatia kupitia kwa watumishi wake, manabii. Israeli wote wamekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii. “Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Torati ya Musa, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu. Kama vile ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa kuacha kutenda dhambi na kuisikiliza kweli yake. Mwenyezi Mungu hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo, hatujamtii. “Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na kujifanyia Jina linalodumu hadi leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako kwa Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka. “Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua za mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu. Ee Mungu, tega sikio, ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”

Shirikisha
Soma Danieli 9