Kumbukumbu la Sheria 31:24-29
Kumbukumbu la Sheria 31:24-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose alipomaliza kuandika maneno ya sheria hiyo tangu mwanzo mpaka mwisho, aliwaambia Walawi, waliokuwa na jukumu la kubeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, “Chukueni kitabu hiki cha sheria, mkiweke karibu na sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili kiwe ushahidi dhidi yenu. Maana najua mlivyo waasi na wakaidi. Ikiwa mmemwasi Mwenyezi-Mungu wakati niko hai pamoja nanyi, itakuwaje baada ya kifo changu? Wakusanye mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maofisa wenu nipate kusema maneno haya wasikie, nazo mbingu na dunia zishuhudie juu yao. Maana ninajua kuwa baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu na kuiacha ile njia niliyowaamuru mwifuate. Na katika siku zijazo mtakumbwa na maafa kwa kuwa mtafanya maovu mbele ya Bwana na kumkasirisha kwa matendo yenu.”
Kumbukumbu la Sheria 31:24-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika kitabu, hata yakaisha, ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la Agano la BWANA akawaambia, Twaeni kitabu hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la Agano la BWANA, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako. Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi ningali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya BWANA; siuze nitakapokwisha kufa! Nikutanishieni wazee wote wa makabila yenu, na maofisa wenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao. Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa BWANA kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu.
Kumbukumbu la Sheria 31:24-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha, ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la agano la BWANA akawaambia, Twaeni chuo hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako. Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi nikali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya BWANA; siuze nitakapokwisha kufa! Nikutanishieni wazee wote wa kabila zenu, na maakida yenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao. Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa BWANA kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu.
Kumbukumbu la Sheria 31:24-29 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya Musa kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho, akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu agizo hili, akawaambia: “Chukueni Kitabu hiki cha Torati mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu. Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Mwenyezi Mungu nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu! Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao. Kwa kuwa ninajua, baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata, kwa sababu mtafanya maovu mbele za macho ya Mwenyezi Mungu, na kuchochea hasira yake kwa kazi za mikono yenu.”