Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 33:12-22

Kumbukumbu la Sheria 33:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Juu ya kabila la Benyamini alisema: “Hili ni kabila alipendalo Mwenyezi-Mungu, nalo hukaa salama karibu naye. Yeye hulilinda mchana kutwa, na kukaa kati ya milima yake.” Juu ya kabila la Yosefu alisema: “Mwenyezi-Mungu na aibariki nchi yake, kwa baraka nzuri kabisa kutoka juu, ibarikiwe kwa matunda bora yalioiva kwa jua, kwa matunda ya kila mwezi; kwa mazao bora ya milima ya kale, na mazao tele ya milima ya kale, Nchi yake ijae yote yaliyo mema, ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu, ambaye alitokea katika kichaka. Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu, aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake. Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza, pembe zake ni za nyati dume. Atazitumia kuyasukuma mataifa; yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia. Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000 na Manase kwa maelfu.” Juu ya kabila la Zebuluni na kabila la Isakari, alisema, “Zebuluni, furahi katika safari zako; nawe Isakari, furahi katika mahema yako. Watawaalika wageni kwenye milima yao, na huko watu watatoa sadaka zinazotakiwa. Maana wao watapata utajiri wao kutoka baharini na hazina zao katika mchanga wa pwani.” Juu ya kabila la Gadi, alisema: “Atukuzwe Mungu ampatiaye Gadi sehemu kubwa. Gadi hunyemelea kama simba akwanyue mkono na utosi wa kichwa. Alijichagulia eneo zuri kuliko yote, mahali ilipotengwa sehemu ya kiongozi. Aliwaongoza watu na kumtii Mwenyezi-Mungu, alitekeleza mpango wa Mungu kwa Israeli.” Juu ya kabila la Dani alisema hivi: “Dani ni mwanasimba arukaye kutoka Bashani.”

Kumbukumbu la Sheria 33:12-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akamnena Benyamini, Mpenzi wa BWANA atakaa salama kwake; Yuamfunika mchana kutwa, Naye hukaa kati ya mabega yake. Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na BWANA; Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande, Na kwa kilindi kilalacho chini, Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, Na kwa vitu vilivyo bora vya mavuno ya miezi, Na kwa vitu viteule vya milima ya kale, Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele, Na kwa vitu vilivyo bora vya nchi, na kujaa kwake, Na uradhi wake aliyekaa ndani ya kile kichaka; Na ije baraka juu ya kichwa chake Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliyetengwa na nduguze. Mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wake mume, enzi ni yake; Na pembe zake ni pembe za nyati; Kwa hizo atayasukuma mataifa yote, hata ncha za nchi; Nao ni makumi ya maelfu ya Efraimu, Nao ni maelfu ya Manase. Na Zabuloni akamnena, Furahi Zabuloni, katika kutoka kwako; Na Isakari, katika hema zako. Watayaita mataifa waje mlimani; Wakasongeze huko sadaka za haki; Kwa kuwa watanyonya wingi wa bahari, Na akiba zilizofichamana za mchangani. Na Gadi akamnena, Na abarikiwe amwongezaye Gadi; Yeye hukaa kama simba mke, Hurarua mkono, naam, na utosi wa kichwa. Akajichagulia sehemu ya kwanza, Kwani ndiko lilikowekwa fungu la mtoa-sheria; Akaja pamoja na wakuu wa watu, Akaitekeleza haki ya BWANA, Na hukumu zake kwa Israeli. Na Dani akamnena, Dani ni mwanasimba, Arukaye kutoka Bashani.

Kumbukumbu la Sheria 33:12-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akamnena Benyamini, Mpenzi wa BWANA atakaa salama kwake; Yuamfunika mchana kutwa, Naye hukaa kati ya mabega yake. Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na BWANA; Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande, Na kwa kilindi kilalacho chini, Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, Na kwa vitu vilivyo bora vya maongeo ya miezi, Na kwa vitu viteule vya milima ya kale, Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele, Na kwa vitu vilivyo bora vya nchi, na kujaa kwake, Na uradhi wake aliyekaa ndani ya kile kijiti; Na ije baraka juu ya kichwa chake Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliyetengwa na nduguze. Mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe wake mume, enzi ni yake; Na pembe zake ni pembe za nyati; Kwa hizo atayasukuma mataifa yote, hata ncha za nchi; Nao ni makumi ya maelfu ya Efraimu, Nao ni maelfu ya Manase. Na Zabuloni akamnena, Furahi Zabuloni, katika kutoka kwako; Na Isakari, katika hema zako. Watayaita mataifa waje mlimani; Wakasongeze huko sadaka za haki; Kwa kuwa watanyonya wingi wa bahari, Na akiba zilizofichamana za mchangani. Na Gadi akamnena, Na abarikiwe amwongezaye Gadi; Yeye hukaa kama simba mke, Hurarua mkono, naam, na utosi wa kichwa. Akajichagulia sehemu ya kwanza, Kwani ndiko lilikowekwa fungu la mtoa-sheria; Akaja pamoja na wakuu wa watu, Akaitekeleza haki ya BWANA, Na hukumu zake kwa Israeli. Na Dani akamnena, Dani ni mwana-simba, Arukaye kutoka Bashani.

Kumbukumbu la Sheria 33:12-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kuhusu Benyamini akasema: “Mwache mpenzi wa BWANA apumzike salama kwake, kwa maana humkinga mchana kutwa, na yule BWANA ampendaye hupumzika kati ya mabega yake.” Kuhusu Yosefu akasema: “BWANA na aibariki nchi yake kwa umande wa thamani kutoka mbinguni juu, na vilindi vya maji vilivyotulia chini; pamoja na vitu vilivyo bora sana viletwavyo na jua, na vitu vizuri sana vinavyoweza kutolewa na mwezi; pamoja na zawadi bora sana za milima ya zamani na kwa wingi wa baraka za vilima vya milele; pamoja na baraka nzuri mno za ardhi na ukamilifu wake, na upendeleo wake yeye aliyeishi kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu, juu ya paji la uso la aliye mkuu miongoni mwa ndugu zake. Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza; pembe zake ni pembe za nyati, na kwa pembe hizo atapiga mataifa, hata yaliyo miisho ya dunia. Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu; hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.” Kuhusu Zabuloni akasema: “Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje, nawe Isakari, katika mahema yako. Watawaita mataifa kwenye mlima, na huko mtatoa dhabihu za haki; watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari, kwa hazina zilizofichwa mchangani.” Kuhusu Gadi akasema: “Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi! Gadi huishi huko kama simba, akirarua kwenye mkono au kichwa. Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote kwa ajili yake mwenyewe; fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa kwa ajili yake. Viongozi wa watu walipokusanyika, alitimiza haki ya mapenzi ya BWANA, na hukumu zake kuhusu Israeli.” Kuhusu Dani akasema: “Dani ni mwana simba, akiruka kutoka Bashani.”