Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 33:12-22

Kumbukumbu 33:12-22 NEN

Kuhusu Benyamini akasema: “Mwache mpenzi wa BWANA apumzike salama kwake, kwa maana humkinga mchana kutwa, na yule BWANA ampendaye hupumzika kati ya mabega yake.” Kuhusu Yosefu akasema: “BWANA na aibariki nchi yake kwa umande wa thamani kutoka mbinguni juu, na vilindi vya maji vilivyotulia chini; pamoja na vitu vilivyo bora sana viletwavyo na jua, na vitu vizuri sana vinavyoweza kutolewa na mwezi; pamoja na zawadi bora sana za milima ya zamani na kwa wingi wa baraka za vilima vya milele; pamoja na baraka nzuri mno za ardhi na ukamilifu wake, na upendeleo wake yeye aliyeishi kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu, juu ya paji la uso la aliye mkuu miongoni mwa ndugu zake. Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza; pembe zake ni pembe za nyati, na kwa pembe hizo atapiga mataifa, hata yaliyo miisho ya dunia. Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu; hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.” Kuhusu Zabuloni akasema: “Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje, nawe Isakari, katika mahema yako. Watawaita mataifa kwenye mlima, na huko mtatoa dhabihu za haki; watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari, kwa hazina zilizofichwa mchangani.” Kuhusu Gadi akasema: “Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi! Gadi huishi huko kama simba, akirarua kwenye mkono au kichwa. Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote kwa ajili yake mwenyewe; fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa kwa ajili yake. Viongozi wa watu walipokusanyika, alitimiza haki ya mapenzi ya BWANA, na hukumu zake kuhusu Israeli.” Kuhusu Dani akasema: “Dani ni mwana simba, akiruka kutoka Bashani.”