Kumbukumbu la Sheria 33:12-22
Kumbukumbu la Sheria 33:12-22 BHN
Juu ya kabila la Benyamini alisema: “Hili ni kabila alipendalo Mwenyezi-Mungu, nalo hukaa salama karibu naye. Yeye hulilinda mchana kutwa, na kukaa kati ya milima yake.” Juu ya kabila la Yosefu alisema: “Mwenyezi-Mungu na aibariki nchi yake, kwa baraka nzuri kabisa kutoka juu, ibarikiwe kwa matunda bora yalioiva kwa jua, kwa matunda ya kila mwezi; kwa mazao bora ya milima ya kale, na mazao tele ya milima ya kale, Nchi yake ijae yote yaliyo mema, ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu, ambaye alitokea katika kichaka. Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu, aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake. Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza, pembe zake ni za nyati dume. Atazitumia kuyasukuma mataifa; yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia. Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000 na Manase kwa maelfu.” Juu ya kabila la Zebuluni na kabila la Isakari, alisema, “Zebuluni, furahi katika safari zako; nawe Isakari, furahi katika mahema yako. Watawaalika wageni kwenye milima yao, na huko watu watatoa sadaka zinazotakiwa. Maana wao watapata utajiri wao kutoka baharini na hazina zao katika mchanga wa pwani.” Juu ya kabila la Gadi, alisema: “Atukuzwe Mungu ampatiaye Gadi sehemu kubwa. Gadi hunyemelea kama simba akwanyue mkono na utosi wa kichwa. Alijichagulia eneo zuri kuliko yote, mahali ilipotengwa sehemu ya kiongozi. Aliwaongoza watu na kumtii Mwenyezi-Mungu, alitekeleza mpango wa Mungu kwa Israeli.” Juu ya kabila la Dani alisema hivi: “Dani ni mwanasimba arukaye kutoka Bashani.”