Kutoka 22:21-31
Kutoka 22:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)
“Msimdhulumu mgeni wala kumtesa, maana nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri. Msimtese mjane au yatima. Kama mkiwadhulumu hao nao wakanililia, hakika nitakisikiliza kilio chao, na hasira yangu itawaka, nami nitawaueni kwa upanga, na wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu yatima. “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni mwa watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba. Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua, kwa kuwa hiyo ndiyo nguo yake ya pekee; ndiyo atakayojifunika nayo. Au wadhani atalalia nini? Akinililia nitamsikiliza, maana mimi ni mwenye huruma. “Usimtukane Mungu, wala kumlaani mkuu wa watu wako. “Usikawie kunitolea sehemu yangu kutokana na wingi wa mazao yako na divai yako. Mtanipa wazaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Mtafanya vivyo hivyo kuhusu wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu. Mtamwacha kila mzaliwa wa kwanza na mama yake kwa siku saba, na siku ya nane mtanitolea. Nyinyi mtakuwa watu waliowekwa wakfu kwangu. Kwa hiyo hamtakula nyama ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini. Nyama hiyo mtawatupia mbwa.
Kutoka 22:21-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema. Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako. Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao wanaume utanipa mimi. Nawe utafanya vivyo hivyo katika ng'ombe wako, na kondoo wako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi. Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yoyote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.
Kutoka 22:21-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yo yote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema. Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako. Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi. Nawe utafanya vivyo katika ng’ombe zako, na kondoo zako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi. Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.
Kutoka 22:21-31 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Usimtendee mgeni vibaya au kumdhulumu, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri. “Usimdhulumu mjane wala yatima. Ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima. “Ukimkopesha mmoja wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. Ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma. “Usimkufuru Mungu au kumlaani mtawala wa watu wako. “Usiache kutoa sadaka kutoka ghala lako au mapipa yako. “Lazima unipe mzaliwa wa kwanza wa wana wako. Ufanye vivyo hivyo kwa ng’ombe wako na kwa kondoo wako. Waache wakae na mama zao kwa siku saba, lakini siku ya nane unipe. “Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.