Ezekieli 14:12-23
Ezekieli 14:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Taifa fulani likitenda dhambi kwa kukosa uaminifu kwangu, mimi nitanyosha mkono wangu kuliadhibu. Nitaiondoa akiba yake ya chakula na kuliletea njaa. Nitawaua watu na wanyama wake. Hata kama Noa, Daneli na Yobu wangalikuwamo nchini humo, wangeyaokoa tu maisha yao wenyewe kwa uadilifu wao. Tena nitapeleka wanyama wa porini katika nchi hiyo na kuwanyanganya watoto wao na kuifanya nchi hiyo kuwa ukiwa, hata hakuna mtu yeyote atakayeweza kupita nchini humo kwa sababu ya wanyama wakali. Hata kama hao watu watatu mashuhuri wangalikuwamo nchini humo, naapa kwa jina langu, mimi Mwenyezi-Mungu, hawangeweza kuwaokoa watoto wao wenyewe; wao wenyewe tu wangeokolewa, lakini nchi hiyo ingekuwa ukiwa. Tena nitazusha vita dhidi ya nchi hiyo na kuamuru itokomezwe na kuulia mbali watu na wanyama. Na kama hao watu watatu wangalikuwamo nchini humo kweli hawangeweza kumwokoa hata mmoja wa watoto wao, wa kiume wala wa kike. Wangeweza tu kuokoa maisha yao wenyewe. Tena nitaleta maradhi mabaya nchini humo na kwa ghadhabu yangu nitawaua watu na wanyama. Na hata kama Noa, Danieli na Yobu wangelikuwa humo, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, kweli hawangeweza kumwokoa hata mtoto wao mmoja wa kiume au wa kike. Wangeyaokoa tu maisha yao wenyewe kwa uadilifu wao. “Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Tena nitauadhibu Yerusalemu kwa mapigo yangu manne ya hukumu kali: Vita, njaa, wanyama wakali na maradhi mabaya, niwatokomeze humo watu na wanyama! Hata hivyo, wakibaki hai watu watakaonusurika na kuwaleta watoto wao wa kiume na wa kike kwako, wewe Ezekieli utaona jinsi walivyo waovu sana; nawe utakubali kwamba adhabu yangu juu ya Yerusalemu ni ya halali. Mienendo na matendo yao vitakuhakikishia kuwa maafa niliyouletea mji huo sikuyaleta bila sababu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 14:12-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuiletea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama; wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU. Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao; wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa. Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama; wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala mabinti; bali wao wenyewe tu wataokoka. Au nikituma tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawangeokoa watoto wa kiume au wa kike; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama? Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na mabinti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake. Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 14:12-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama; wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU. Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao; wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa. Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama; wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; bali wao wenyewe tu wataokoka. Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama? Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na binti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake. Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 14:12-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema, “Mwanadamu, nchi ikinitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikaunyoosha mkono wangu dhidi yake ili kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, hata kama watu hawa watatu: Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, wangeweza kujiokoa hao wenyewe tu kwa uadilifu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi. “Au nikiwaachilia wanyama pori katika nchi hiyo nao wakaiacha bila watoto, nayo ikawa ukiwa hivi kwamba hakuna mtu apitaye kwa sababu ya wanyama pori, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa. “Au nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikaua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa. “Au nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kupitia kumwaga damu, kuua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao. “Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! Lakini patakuwa na watakaookoka: wana wa kiume na wa kike watakaoletwa kutoka nchi hiyo. Watakuja kwenu, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya maafa yale yote niliyoleta juu yake. Mtafarijika mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwani mtajua kuwa sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”