Wagalatia 3:15-18
Wagalatia 3:15-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.
Wagalatia 3:15-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazawa, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa njia ya ahadi.
Wagalatia 3:15-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.
Wagalatia 3:15-18 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. Ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa uzao”, yakimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako”, yaani mtu mmoja, ndiye Al-Masihi. Ninachotaka kusema ni kwamba, Torati, ambayo ilitolewa miaka mia nne na thelathini (430) baadaye, haitangui agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. Kwa maana kama urithi hupatikana kwa Torati, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Ibrahimu urithi kupitia kwa ahadi.