Mwanzo 35:1-15
Mwanzo 35:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.” Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu. Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.” Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu. Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia. Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao. Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake. Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi. Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli. Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme. Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.” Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu. Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta. Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli.
Mwanzo 35:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na vipuli vilivyokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo. Basi Yakobo akafika Luzu, katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye. Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake. Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi. Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka katika uzao wako. Na nchi hii niliyowapa Abrahamu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo. Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye. Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake. Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli.
Mwanzo 35:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo. Basi Yakobo akafika Luzu, ulio katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye. Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake. Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi. Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako. Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo. Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye. Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake. Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli.
Mwanzo 35:1-15 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko. Ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.” Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mjitakase na mkabadilishe nguo zenu. Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipoenda.” Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mwaloni ulio Shekemu. Kisha wakaondoka, na utisho wa Mungu ukaipata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo. Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani. Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alijifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake. Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mwaloni ulio nje ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi. Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo. Lakini hutaitwa tena Yakobo; jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli. Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako. Nchi niliyowapa Ibrahimu na Isaka nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.” Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye. Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake. Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.