Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 35

35
Yakobo arudi Betheli
1Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko. Ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”
2Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mjitakase na mkabadilishe nguo zenu. 3Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipoenda.” 4Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mwaloni ulio Shekemu. 5Kisha wakaondoka, na utisho wa Mungu ukaipata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.
6Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani. 7Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli#35:7 maana yake Mungu wa Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alijifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
8Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mwaloni ulio nje ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi#35:8 maana yake Mwaloni wa kilio.
9Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. 10Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo#35:10 maana yake Ashikaye kisigino, au Atwaaye mahali pa mwingine, au Mdanganyaji. Lakini hutaitwa tena Yakobo; jina lako litakuwa Israeli#35:10 maana yake Yeye ashindanaye na Mungu.” Kwa hiyo akamwita Israeli.
11Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi#35:11 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).; ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako. 12Nchi niliyowapa Ibrahimu na Isaka nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.” 13Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.
14Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake. 15Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli#35:15 maana yake Nyumba ya Mungu.
Vifo vya Raheli na Isaka
16Kisha wakaondoka Betheli. Kabla hawajafika Efrata, Raheli akaanza kujifungua na akapata shida kuu. 17Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.” 18Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe jina Benoni#35:18 maana yake Mwana wa huzuni yangu. Lakini babaye akamwita jina Benyamini#35:18 maana yake Mwana wa mkono wangu wa kuume.
19Kwa hiyo Raheli akafa, na akazikwa kando ya njia iendayo Efrata (ndio Bethlehemu). 20Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ambayo hadi leo inatambulisha kaburi la Raheli.
21Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema baada ya kupita Mnara wa Ederi. 22Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aliyeitwa Bilha, naye Israeli akasikia jambo hilo.
Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:
23Wana wa Lea walikuwa:
Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo,
Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.
24Wana wa Raheli walikuwa:
Yusufu na Benyamini.
25Wana waliozaliwa na Bilha mjakazi wa Raheli walikuwa:
Dani na Naftali.
26Wana waliozaliwa na Zilpa mjakazi wa Lea walikuwa:
Gadi na Asheri.
Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.
27Yakobo akarudi nyumbani mwa baba yake Isaka huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Ibrahimu na Isaka. 28Isaka aliishi miaka mia moja na themanini. 29Kisha Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho, akafa; akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee aliyeshiba siku. Nao Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 35: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia