Hosea 10:1-15
Hosea 10:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walikuwa kama mzabibu mzuri, mzabibu wenye kuzaa matunda. Kadiri matunda yalivyozidi kuongezeka, ndivyo walivyozidi kujijengea madhabahu. Kadiri nchi yao ilivyozidi kustawi, ndivyo walivyozidi kupamba nguzo zao za ibada. Mioyo yao imejaa udanganyifu. Sasa ni lazima wawajibike kwa hatia yao. Mwenyezi-Mungu atazibomoa madhabahu zao na kuziharibu nguzo zao. Wakati huo watasema: “Hatuna tena mfalme, kwa kuwa hatumchi Mwenyezi-Mungu; lakini, naye mfalme atatufanyia nini?” Wanachosema ni maneno matupu; wanaapa na kufanya mikataba ya bure; haki imekuwa si haki tena, inachipua kama magugu ya sumu shambani. Wakazi wa Samaria watatetemeka kwa sababu ya ndama wa huko Betheli. Watu wake watamwombolezea ndama huyo, hata makuhani wanaomwabudu watamlilia; kwani fahari ya ndama huyo imeondolewa. Kinyago hicho kitapelekwa Ashuru, kama ushuru kwa mfalme mkuu. Watu wa Efraimu wataaibishwa, Waisraeli watakionea aibu kinyago chao. Mfalme wa Samaria atachukuliwa, kama kipande cha mti juu ya maji. Mahali pa kuabudia vilimani pa Aweni, dhambi ya Waisraeli, pataharibiwa. Miiba na magugu vitamea katika madhabahu zao. Nao wataiambia milima, “Tufunikeni” na vilima, “Tuangukieni!” Enyi Waisraeli, nyinyi mmetenda dhambi tangu kule Gibea, na bado mnaendelea. Hakika vita vitawaangamiza hukohuko Gibea. Nitawajia watu hawa wapotovu na kuwaadhibu; watu wa mataifa watakusanyika kuwashambulia, watakapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao nyingi. Efraimu ni ndama aliyefundishwa vizuri, akapenda kupura nafaka. Lakini sasa shingo yake nzuri nitaifunga nira. Yuda atalima kwa jembe yeye mwenyewe, naam, Yakobo atakokota jembe la kupalilia. Pandeni wema kwa faida yenu, nanyi mtavuna upendo; limeni mashamba yaliyoachwa, maana wakati wa kunitafuta mimi Bwana umefika nami nitawanyeshea baraka. Lakini nyinyi mmepanda uovu, nyinyi mmevuna dhuluma; mmekula matunda ya uongo wenu. Wewe Israeli ulitegemea nguvu zako mwenyewe, na wingi wa askari wako. Kwa hiyo msukosuko wa vita utawajia watu wako; ngome zako zote zitaharibiwa, kama Shalmani alivyoharibu Beth-arbeli vitani, kina mama wakapondwa pamoja na watoto wao. Ndivyo itakavyokuwa kwenu enyi watu wa Betheli, kwa sababu ya uovu wenu mkuu. Kutakapopambazuka mfalme wa Israeli atawatokomeza.
Hosea 10:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Israeli ni mzabibu mzuri, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri. Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao. Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi BWANA; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini? Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba. Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka. Nayo itachukuliwa Ashuru, iwe zawadi kwa mfalme Yarebu; Efraimu atapata aibu, na Israeli atalionea haya shauri lake mwenyewe. Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji. Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni. Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; Je, vita juu ya wana wa uovu hakitawapata katika Gibea? Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili. Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atapiga haro yeye mwenyewe. Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki. Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako. Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjikavunjika pamoja na watoto wake. Hivyo ndivyo Betheli atakavyowatenda ninyi, kwa sababu ya ubaya wenu mwingi; wakati wa mapambazuko mfalme wa Israeli atakatiliwa mbali kabisa.
Hosea 10:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri. Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao. Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi BWANA; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini? Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba. Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-Aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka. Nayo itachukuliwa Ashuru, iwe zawadi kwa mfalme Yarebu; Efraimu atapata aibu, na Israeli atalionea haya shauri lake mwenyewe. Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji. Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni. Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; ili vita vilivyokuwa juu ya wana wa uovu visiwapate katika Gibea. Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili. Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atavunja madongoa yake. Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki. Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako. Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjika-vunjika pamoja na watoto wake. Hivyo ndivyo Betheli atakavyowatenda ninyi, kwa sababu ya ubaya wenu mwingi; wakati wa mapambazuko mfalme wa Israeli atakatiliwa mbali kabisa.
Hosea 10:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana, alijizalia matunda mwenyewe. Kadiri matunda yake yalivyoongezeka, alijenga madhabahu zaidi; kadiri nchi yake ilivyostawi, alipamba mawe yake ya ibada. Moyo wao ni mdanganyifu, nao sasa lazima wachukue hatia yao. BWANA atabomoa madhabahu zao na kuharibu mawe yao ya ibada. Kisha watasema, “Hatuna mfalme kwa sababu hatukumheshimu BWANA. Lakini hata kama tungelikuwa na mfalme, angeweza kutufanyia nini?” Wanaweka ahadi nyingi, huapa viapo vya uongo wanapofanya mapatano; kwa hiyo mashtaka huchipuka kama magugu ya sumu katika shamba lililolimwa. Watu wanaoishi Samaria huogopa kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni. Watu wake wataiombolezea, vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu, wale waliokuwa wamefurahia fahari yake, kwa sababu itaondolewa kutoka kwao kwenda uhamishoni. Itachukuliwa kwenda Ashuru kama ushuru kwa mfalme mkuu. Efraimu atafedheheshwa; Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti. Samaria na mfalme wake wataelea kama kijiti juu ya uso wa maji. Mahali pa kuabudia sanamu pa uovu pataharibiwa: ndiyo dhambi ya Israeli. Miiba na mibaruti itaota na kufunika madhabahu zao. Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!” na vilima, “Tuangukieni!” “Tangu siku za Gibea, mmetenda dhambi, ee Israeli, huko ndiko mlikobaki. Je, vita havikuwapata watenda mabaya huko Gibea? Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu; mataifa yatakusanywa dhidi yao ili kuwaweka katika vifungo kwa ajili ya dhambi zao mbili. Efraimu ni mtamba wa ngʼombe aliyefundishwa ambaye hupenda kupura, hivyo nitamfunga nira juu ya shingo yake nzuri. Nitamwendesha Efraimu, Yuda lazima alime, naye Yakobo lazima avunjavunje mabonge ya udongo. Jipandieni wenyewe haki, vuneni matunda ya upendo usio na kikomo, vunjeni ardhi yenu isiyolimwa; kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta BWANA, mpaka atakapokuja na kuwanyeshea juu yenu haki. Lakini mmepanda uovu, mkavuna ubaya, mmekula tunda la udanganyifu. Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe na wingi wa mashujaa wenu, mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako, ili kwamba ngome zako zote zitaharibiwa: kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita, wakati mama pamoja na watoto wao walipotupwa kwa nguvu ardhini. Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli, kwa sababu uovu wako ni mkuu. Siku ile itakapopambazuka, mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.