Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 10

10
Kuharibiwa kwa vitu vya ibada vya Israeli
1Waisraeli walikuwa kama mzabibu mzuri,
mzabibu wenye kuzaa matunda.
Kadiri matunda yalivyozidi kuongezeka,
ndivyo walivyozidi kujijengea madhabahu.
Kadiri nchi yao ilivyozidi kustawi,
ndivyo walivyozidi kupamba nguzo zao za ibada.
2Mioyo yao imejaa udanganyifu.
Sasa ni lazima wawajibike kwa hatia yao.
Mwenyezi-Mungu atazibomoa madhabahu zao
na kuziharibu nguzo zao.
3Wakati huo watasema:
“Hatuna tena mfalme,
kwa kuwa hatumchi Mwenyezi-Mungu;
lakini, naye mfalme atatufanyia nini?”
4Wanachosema ni maneno matupu;
wanaapa na kufanya mikataba ya bure;
haki imekuwa si haki tena,
inachipua kama magugu ya sumu shambani.
5Wakazi wa Samaria watatetemeka
kwa sababu ya ndama wa huko Betheli.
Watu wake watamwombolezea ndama huyo,
hata makuhani wanaomwabudu watamlilia;
kwani fahari ya ndama huyo imeondolewa.
6Kinyago hicho kitapelekwa Ashuru,
kama ushuru kwa mfalme mkuu.
Watu wa Efraimu wataaibishwa,
Waisraeli watakionea aibu kinyago chao.
7Mfalme wa Samaria atachukuliwa,
kama kipande cha mti juu ya maji.
8Mahali pa kuabudia vilimani pa Aweni,
dhambi ya Waisraeli, pataharibiwa.
Miiba na magugu vitamea katika madhabahu zao.
Nao wataiambia milima, “Tufunikeni”
na vilima, “Tuangukieni!”
Israeli atavuna alichopanda
9Enyi Waisraeli,
nyinyi mmetenda dhambi tangu kule Gibea,
na bado mnaendelea.
Hakika vita vitawaangamiza hukohuko Gibea.
10Nitawajia watu hawa wapotovu na kuwaadhibu;
watu wa mataifa watakusanyika kuwashambulia,
watakapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao nyingi.
11Efraimu ni ndama aliyefundishwa vizuri,
akapenda kupura nafaka.
Lakini sasa shingo yake nzuri nitaifunga nira.
Yuda atalima kwa jembe yeye mwenyewe,
naam, Yakobo atakokota jembe la kupalilia.
12Pandeni wema kwa faida yenu,
nanyi mtavuna upendo;
limeni mashamba yaliyoachwa,
maana wakati wa kunitafuta mimi Bwana umefika
nami nitawanyeshea baraka.
13Lakini nyinyi mmepanda uovu,
nyinyi mmevuna dhuluma;
mmekula matunda ya uongo wenu.
Wewe Israeli ulitegemea nguvu zako mwenyewe,
na wingi wa askari wako.
14Kwa hiyo msukosuko wa vita utawajia watu wako;
ngome zako zote zitaharibiwa,
kama Shalmani alivyoharibu Beth-arbeli vitani,
kina mama wakapondwa pamoja na watoto wao.
15Ndivyo itakavyokuwa kwenu enyi watu wa Betheli,
kwa sababu ya uovu wenu mkuu.
Kutakapopambazuka mfalme wa Israeli atawatokomeza.

Iliyochaguliwa sasa

Hosea 10: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia