Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 11

11
Upendo wa Mungu wapita hasira yake
1“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda,
Kutoka Misri nilimwita mwanangu.
2Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita,
ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami;
waliendelea kuyatambikia Mabaali,
na kuvifukizia ubani vinyago vya miungu.
3Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea!
Mimi mwenyewe niliwachukua mikononi mwangu;
lakini hawakutambua kuwa mimi ndiye niliyewatunza.
4Niliwaongoza kwa kamba za huruma
naam, kwa kamba za upendo;
kama baba amwinuaye mtoto mpaka shavuni mwake,
ndivyo nami nilivyokuwa kwao.
Mimi niliinama chini na kuwalisha.
5Basi, watarudi nchini Misri;
watatawaliwa na mfalme wa Ashuru,
kwa sababu wamekataa kunirudia.
6“Upanga utavuma katika miji yao,
utavunjavunja miimo ya malango yake
na kuwaangamiza katika ngome zao.
7Watu wangu wamepania kuniacha mimi,
wakiitwa waje juu,
hakuna hata mmoja anayeweza.#11:7 maana ya mistari hii miwili katika Kiebrania si dhahiri.
8Ewe Efraimu, nawezaje kukuacha?
Nawezaje kukutupa ewe Israeli?
Nitawezaje kukufanya kama mji wa Adma?
Nitawezaje kukutenda kama Seboimu!
Nazuiwa na moyo wangu;
huruma yangu imezidi kuwa motomoto.
9Nitaizuia hasira yangu kali;
sitamwangamiza tena Efraimu,
maana mimi ni Mungu, wala si binadamu.
“Mimi ndimi Mtakatifu miongoni mwenu,
nami sitakuja kuwaangamiza.
10“Watanifuata mimi Mwenyezi-Mungu ningurumaye kama simba;
nitakaponguruma watanijia toka magharibi wakitetemeka.
11Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege,
wataruka kutoka Ashuru kama hua
nami nitawarudisha makwao;
mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12Watu wa Efraimu wananirundikia uongo,
na Waisraeli udanganyifu.
Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu.

Iliyochaguliwa sasa

Hosea 11: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia