Isaya 18:1-7
Isaya 18:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole, wake nchi iliyojaa mvumo wa mabawa, nchi iliyoko ngambo ya mito ya Kushi! Inatuma wajumbe ambao wanasafiri mtoni Nili, wamepanda mashua za mafunjo. Nendeni, enyi wajumbe wepesi, kwa taifa kubwa na hodari, la watu warefu na wa ngozi laini. Watu hao wanaoogopwa kila mahali na nchi yao imegawanywa na mito. Enyi wakazi wote ulimwenguni, nanyi mkaao duniani! Ishara itakapotolewa mlimani, tazameni! Tarumbeta itakapopigwa, sikilizeni. Maana, Mwenyezi-Mungu ameniambia hivi: “Toka makao yangu juu nitatazama yanayotukia, nimetulia kama joto katika mwanga wa jua, kama wingu la umande wakati wa mavuno. Maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua umekwisha, maua yamepukutika na kuwa zabibu mbivu, Mungu atakata chipukizi kwa kisu cha kupogolea, na kuyakwanyua matawi yanayotanda. Yote yataachiwa ndege milimani, na wanyama wengine wa porini. Ndege walao nyama watakaa humo wakati wa majira ya kiangazi, na wanyama wa porini watafanya makao humo wakati wa majira ya baridi.” Wakati huo, Mwenyezi-Mungu wa majeshi ataletewa tambiko kutoka kwa watu warefu wenye ngozi laini, watu watishao karibu na mbali, taifa la watu wenye nguvu na ushindi, ambalo ardhi yake imegawanywa na mito. Ataletewa tambiko hizo mlimani Siyoni anapoabudiwa yeye Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Isaya 18:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa, Iliyoko mbali kupita mito ya Kushi; Ipelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari, Na katika vyombo vya manyasi juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao. Enyi watu mkaao katika ulimwengu wote, na wenyeji wa dunia, bendera ikiinuliwa milimani, angalieni; na wakipiga tarumbeta, sikieni. Maana BWANA ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa jua kali, mfano wa wingu la umande katika joto la mavuno. Maana kabla ya mavuno, maua yaangukapo, na maua yakawa zabibu zianzazo kuiva, ndipo atakapoyakata matawi kwa miundu, na kuviondoa vitawi vilivyopanuka na kuvikata. Wote pamoja wataachiwa ndege wakali wa milimani, na wanyama wa nchi; ndege wakali watakaa juu yao wakati wa jua, na wanyama wote wa nchi watakaa juu yao wakati wa baridi. Wakati huo BWANA wa majeshi ataletewa hidaya na watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inagawanya nchi yao; Mpaka mahali pa jina la BWANA wa majeshi, mlima Sayuni.
Isaya 18:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa, Iliyoko mbali kupita mito ya Kushi; Ipelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari, Na katika vyombo vya manyasi juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao. Enyi watu mkaao katika ulimwengu wote, na wenyeji wa dunia, bendera ikiinuliwa milimani, angalieni; na wakipiga tarumbeta, sikieni. Maana BWANA ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa jua kali, mfano wa wingu la umande katika hari ya mavuno. Maana kabla ya mavuno, maua yaangukapo, na maua yakawa zabibu zianzazo kuiva, ndipo atakapoyakata matawi kwa miundu, na kuviondoa vitawi vilivyopanuka na kuvikata. Wote pamoja wataachiwa ndege wakali wa milimani, na hayawani wa nchi; ndege wakali watakaa juu yao wakati wa jua, na hayawani wote wa nchi watakaa juu yao wakati wa baridi. Wakati huo BWANA wa majeshi ataletewa hedaya na watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao; Mpaka mahali pa jina la BWANA wa majeshi, mlima Sayuni.
Isaya 18:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa, kando ya mito ya Kushi, iwapelekayo wajumbe wake kupitia bahari kwa mashua za mafunjo juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito. Enyi mataifa yote ya ulimwengu, ninyi mnaoishi duniani wakati bendera itakapoinuliwa milimani, mtaiona, nayo tarumbeta itakapolia, mtaisikia. Hili ndilo BWANA aliloniambia: “Nitatulia kimya na kutazama kutoka maskani yangu, kama joto linalometameta katika mwanga wa jua, kama wingu la umande katika joto la wakati wa mavuno.” Kwa maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua ukishapita na maua yakawa zabibu zinazoiva, atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi, naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka. Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani na wanyama pori, ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi, nao wanyama pori wakati wote wa masika. Wakati huo matoleo yataletwa kwa BWANA wa majeshi kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito, matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la BWANA wa majeshi.