Yobu 24:1-12
Yobu 24:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mbona Mungu Mwenye Nguvu haweki wakati maalumu wa hukumu; au kwa nini wamjuao hawazijui siku hizo zake? Watu wanaoondoa alama za mipaka ya mashamba, na wengine huiba mifugo na kuilisha. Huwanyanganya yatima punda wao, humweka rehani ng'ombe wa mjane. Huwasukuma maskini kando ya barabara; maskini wa dunia hujificha mbele yao. Kwa hiyo kama pundamwitu maskini hutafuta chakula jangwani wapate chochote cha kuwalisha watoto wao. Maskini wanalazimika kuokota mabaki ya mavuno mashambani, wanaokota katika mashamba ya mizabibu ya waovu. Usiku kucha hulala uchi bila nguo wakati wa baridi hawana cha kujifunikia. Wamelowa kwa mvua ya milimani, hujibanza miambani kujificha wasilowe. Wapo na wanaowanyakua watoto yatima vifuani mwa mama yao. Wengine huwaweka rehani watoto wa maskini. Watoto hao hufanywa waende uchi bila nguo, wakivuna ngano huku njaa imewabana, wakiwatengenezea waovu mafuta yao, au kukamua divai bila hata kuionja. Kutoka mjini kilio cha wanaokufa chasikika, na walioumizwa hupaza sauti kuomba msaada; lakini Mungu hasikilizi kabisa sala zao.
Yobu 24:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi? Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake? Wako waziondoao alama za mipaka; Huyachukua makundi na kuyalisha. Huwanyang'anya yatima punda wao, Humtwaa rehani ng'ombe wake mwanamke mjane. Humgeuza mhitaji aiache njia; Maskini wa nchi hujificha pamoja. Tazama, kama punda mwitu jangwani Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii; Jangwa huwapa chakula cha watoto wao. Hukata nafaka zao mashambani; Na kuokota zabibu za waovu. Hujilaza usiku kucha uchi bila nguo, Wala hawana cha kujifunika baridi. Hutota kwa manyunyu ya milimani, Na kugandamania kwa jabali ili kujikinga, Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba, Na kutwaa rehani kwa maskini; Hata wazunguke uchi bila mavazi, Nao wakiwa na njaa huchukua miganda; Hushindika mafuta ndani ya kuta za watu hao; Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu. Watu huugua toka mji ulio na watu wengi, Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele; Wala Mungu hauangalii upumbavu.
Yobu 24:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi? Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake? Wako waziondoao alama za mipaka; Huyachukua makundi kwa jeuri na kuyalisha. Humfukuza punda wake asiye baba, Humtwaa rehani ng’ombe wake mwanamke mjane. Humgeuza mhitaji aiache njia; Maskini wa nchi hujificha pamoja. Tazama, kama punda-mwitu jangwani Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii; Jangwa huwapa chakula cha watoto wao. Hukata nafaka zao mashambani; Na kuokota zabibu za waovu. Hujilaza usiku kucha uchi pasipo nguo, Wala hawana cha kujifunika baridi. Hutota kwa manyunyo ya milimani, Na kuambatana na jabali kwa kukosa sitara, Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba, Na kutwaa rehani kwa maskini; Hata wazunguke uchi pasipo mavazi, Nao wakiwa na njaa huchukua miganda; Hushindika mafuta ndani ya makuta ya watu hao; Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu. Watu huugua toka mji ulio na watu wengi, Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele; Wala Mungu hauangalii upumbavu.
Yobu 24:1-12 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu? Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio? Watu husogeza mawe ya mpaka; huchunga makundi ya wanyama waliyonyang’anya kwa nguvu. Huwanyang’anya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane. Humsukuma mhitaji kutoka njia, na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha. Kama punda-mwitu jangwani, maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula; mahali palipo jangwa huwapa chakula cha watoto wao. Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo katika mashamba ya mizabibu ya waovu. Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi; hawana chochote cha kujifunika baridi. Hutota kwa mvua za mlimani, nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri. Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto mchanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni. Kwa kukosa nguo, hutembea uchi; hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa. Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia; hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu. Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya.