Yobu 3:1-10
Yobu 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Hatimaye Yobu aliamua kuongea, akailaani siku aliyozaliwa. Yobu akasema: “Ilaaniwe siku ile niliyozaliwa; usiku ule iliposemwa, ‘Mwana amechukuliwa mimba’ Siku hiyo na iwe giza! Mungu juu asijishughulishe nayo! Wala nuru yoyote isiiangaze! Mauzauza na giza nene yaikumbe, mawingu mazito yaifunike. Giza la mchana liitishe! Usiku huo giza nene liukumbe! Usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usitiwe katika idadi ya siku za mwezi. Naam, usiku huo uwe tasa, sauti ya furaha isiingie humo. Walozi wa siku waulaani, watu stadi wa kuligutua dude Lewiyathani waulaani! Nyota zake za pambazuko zififie, utamani kupata mwanga, lakini usipate, wala usione nuru ya pambazuko. Maana usiku huo haukulifunga tumbo la mama, wala kuficha taabu nisizione.
Yobu 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto wa kiume ametungishwa mimba. Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo Lewiathani. Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone mapambazuko; Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni.
Yobu 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani. Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi; Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni.
Yobu 3:1-10 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake. Kisha akasema: “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali, na usiku ule iliposemekana, ‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’ Siku ile na iwe giza; Mungu juu na asiiangalie; nayo nuru isiiangazie. Giza na kivuli kikuu viikalie tena; wingu na likae juu yake; weusi na uifunike nuru yake. Usiku ule na ushikwe na giza nene; usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote. Usiku ule na uwe tasa; sauti ya furaha na isisikike ndani yake. Wale wanaozilaani siku na wailaani hiyo siku, wale walio tayari kumwamsha Lewiathani. Nyota zake za alfajiri na ziwe giza; nao ungojee mwanga bila mafanikio, wala usiione miali ya mapambazuko, kwa sababu huo usiku haukunifungia mlango wa tumbo la mama yangu, ili kuyaficha macho yangu kutokana na taabu.