Ayubu 3
3
Sehemu ya pili: Mazungumzo ya Ayubu na rafiki zake watatu
(Ayubu 3–31)
Hotuba ya kwanza ya Ayubu
Ayubu anailaani siku aliyozaliwa
1Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.
2Kisha akasema:
3“Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,
na usiku ule iliposemekana,
‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
4Siku ile na iwe giza;
Mungu juu na asiiangalie;
nayo nuru isiiangazie.
5Giza na kivuli kikuu viikalie tena;
wingu na likae juu yake;
weusi na uifunike nuru yake.
6Usiku ule na ushikwe na giza nene;
usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.
7Usiku ule na uwe tasa;
sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
8Wale wanaozilaani siku na wailaani hiyo siku,
wale walio tayari kumwamsha Lewiathani#3:8 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa..
9Nyota zake za alfajiri na ziwe giza;
nao ungojee mwanga bila mafanikio,
wala usiione miali
ya mapambazuko,
10kwa sababu huo usiku haukunifungia
mlango wa tumbo la mama yangu,
ili kuyaficha macho yangu
kutokana na taabu.
11“Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?
Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
12Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea
na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
13Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani.
Ningekuwa nimelala na kupumzika
14pamoja na wafalme na washauri wa dunia,
waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,
15pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,
waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
16Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu,
kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?
17Huko waovu huacha kusumbua
na huko waliochoka hupumzika.
18Wafungwa nao hufurahia utulivu wao,
hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.
19Wadogo kwa wakubwa wamo humo,
na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.
20“Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni,
na hao wenye uchungu kupewa uhai,
21wale wanaotamani kifo ambacho hakiji,
wale wanaotafuta kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
22ambao hujawa na furaha,
na hushangilia wanapofika kaburini?
23Kwa nini uhai hupewa mtu
ambaye njia yake imefichika,
ambaye Mungu amemzingira?
24Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula;
kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.
25Lile nililokuwa nikiogopa limenijia;
lile nililokuwa nikihofia limenipata.
26Sina amani, wala utulivu;
sina pumziko, bali taabu tu.”
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.