Yobu 38:25-38
Yobu 38:25-38 Biblia Habari Njema (BHN)
“Nani aliyechora angani njia kwa ajili ya mvua? Nani aliyeionesha radi njia yake mawinguni, ikasababisha mvua kunyesha nchini kusikoishi mtu na jangwani ambako hakuna mtu, ili kuiburudisha nchi kavu na kame na kuifanya iote nyasi? “Je, mvua ina baba? Au nani ameyazaa matone ya umande? Je, barafu ilitoka tumboni kwa nani? Nani aliyeizaa theluji? Maji hugeuka kuwa magumu kama jiwe, na uso wa bahari ukaganda. “Angalia makundi ya nyota: Je, unaweza kuifunga minyororo Kilimia, au kuvilegeza vifungo vya Orioni? Je, waweza kuziongoza nyota katika majira yake, au kumwongoza Dubu pamoja na watoto wake? Je, wazijua kanuni zinazotawala mbingu; Je, waweza kuzipangia taratibu zao duniani? “Je, waweza kupaza sauti na kuyaamuru mawingu yakufunike kwa mtiririko wa mvua? Je, wewe ukiamuru umeme umulike, utakujia na kusema: ‘Nipo hapa?’ Ni nani aliyemjulisha kwarara kujaa kwa mto Nili au aliyemwambia jogoo kwamba mvua inakuja? Nani mwenye akili ya kuweza kuhesabu mawingu, au kuinamisha viriba vya maji huko mbinguni? ili vumbi duniani igandamane na udongo ushikamane na kuwa matope?
Yobu 38:25-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, Au njia kwa umeme wa radi; Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo? Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa? Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi. Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni? Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake? Je! Unazijua amri zilizoamriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa? Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja?
Yobu 38:25-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, Au njia kwa umeme wa radi; Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo? Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa? Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi. Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni? Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake? Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa? Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja?
Yobu 38:25-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi na njia ya umeme wa radi, ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu, jangwa lisilo na yeyote ndani yake, ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa, na majani yaanze kumea ndani yake? Je, mvua ina baba? Ni nani baba azaaye matone ya umande? Barafu inatoka tumbo la nani? Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni, wakati maji yawapo magumu kama jiwe, wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda? “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia? Waweza kulegeza kamba za Orioni? Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake, au kuongoza Dubu na watoto wake? Je, unajua sheria zinazotawala mbingu? Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani? “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji? Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake? Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’? Ni nani aliyeujalia moyo hekima au kuzipa akili ufahamu? Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu? Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni wakati mavumbi yawapo magumu, na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?