Yobu 42:10-17
Yobu 42:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya Yobu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi-Mungu akamrudishia Yobu hali yake ya kwanza. Alimpa maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali. Kisha ndugu zake, dada zake na rafiki wote waliomfahamu hapo awali wakamwendea nyumbani kwake, wakala chakula pamoja naye. Wakampa pole na kumfariji kwa ajili ya mateso yote ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemletea. Kila mmoja wao akampa Yobu fedha na pete ya dhahabu. Katika miaka ya Yobu iliyofuata Mwenyezi-Mungu alimbariki zaidi kuliko hata alivyokuwa amembariki pale awali. Basi Yobu akawa na kondoo 14,000, ngamia 6,000, ng'ombe 2,000 na punda majike 1,000. Alikuwa pia na watoto wa kiume saba na wa kike watatu. Binti yake wa kwanza alimpa jina Yemima, wa pili Kezia, na wa mwisho Keren-hapuki. Katika nchi yote hiyo hapakuwa na wanawake waliokuwa wazuri kama mabinti wa Yobu. Baba yao akawaachia urithi kama alivyowaachia kaka zao. Baada ya hapo, Yobu aliishi miaka 140, akawaona wajukuu na vitukuu vyake vyote hadi kizazi cha nne. Basi, Yobu akafariki akiwa mzee wa miaka mingi.
Yobu 42:10-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akamrejeshea Ayubu mali yake, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea ndugu zake wote, wanaume kwa wanawake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakampa pole na kumliwaza kwa ajili ya mateso hayo yote aliyoleta BWANA juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo BWANA akaubariki huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu moja, na punda wake elfu moja. Tena alikuwa na watoto wa kiume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao wa kiume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia moja na arubaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hadi kizazi cha nne. Basi Ayubu akafa, akiwa mzee sana mwenye kujawa na siku.
Yobu 42:10-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote BWANA aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.
Yobu 42:10-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, BWANA akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni. Ndipo ndugu zake wote waume kwa wake na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni, wakaja wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote BWANA aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu. BWANA akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda wa kike elfu moja. Tena alikuwa na wana saba na binti watatu. Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia na wa tatu Keren-Hapuki. Hapakuwepo mahali popote katika nchi ile yote palipopatikana wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao. Baada ya hili Ayubu akaishi miaka 140; akawaona wanawe na wana wa wanawe hata kizazi cha nne. Hivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyekuwa ameshiba siku.