Yoeli 3:14-21
Yoeli 3:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Wanafika makundi kwa makundi kwenye bonde la Hukumu, maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia. Jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu ananguruma huko Siyoni; sauti yake inavuma kutoka Yerusalemu; mbingu na dunia vinatetemeka. Lakini Mwenyezi-Mungu ni kimbilio la watu wake, ni ngome ya usalama kwa Waisraeli. “Hapo, ewe Israeli, utajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nakaa Siyoni, mlima wangu mtakatifu, Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu; na wageni hawatapita tena humo. “Wakati huo, milima itatiririka divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa. Vijito vyote vya Yuda vitajaa maji; chemchemi itatokea nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, na kulinywesha bonde la Shitimu. “Misri itakuwa mahame, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu waliwashambulia watu wa Yuda wakawaua watu wasio na hatia. Bali Yuda itakaliwa milele, na Yerusalemu kizazi hata kizazi. Nitawaadhibu waliomwaga damu ya watu wa Yuda wala sitawaachia wenye hatia. Mimi, Mwenyezi-Mungu nakaa Siyoni.”
Yoeli 3:14-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Umati mkubwa, umati mkubwa, wamo katika bonde la kukata kauli! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata kauli. Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Naye BWANA atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka; lakini BWANA atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli. Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe. Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya BWANA, na kulinywesha bonde la Shitimu. Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao. Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi. Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana BWANA ndiye akaaye Sayuni.
Yoeli 3:14-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata maneno. Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Naye BWANA atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka; lakini BWANA atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli. Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe. Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya BWANA, na kulinywesha bonde la Shitimu. Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao. Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi. Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana BWANA ndiye akaaye Sayuni.
Yoeli 3:14-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Umati mkubwa, umati mkubwa katika bonde la uamuzi! Kwa kuwa siku ya BWANA ni karibu katika bonde la uamuzi. Jua na mwezi vitatiwa giza, na nyota hazitatoa mwanga wake tena. BWANA atanguruma kutoka Sayuni na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu; dunia na mbingu vitatikisika. Lakini BWANA atakuwa kimbilio la watu wake, ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli. “Ndipo mtakapojua kwamba Mimi, BWANA Mungu wenu, nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Yerusalemu utakuwa mtakatifu; kamwe wageni hawatavamia tena. “Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa; mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji. Chemchemi itatiririka kutoka kwenye nyumba ya BWANA na kunywesha Bonde la Shitimu. Lakini Misri itakuwa ukiwa, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda, ambao katika nchi yao walimwaga damu isiyo na hatia. Yuda itakaliwa na watu milele na Yerusalemu itadumu vizazi vyote. Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe, nitasamehe.”