Yoeli 3:14-21
Yoeli 3:14-21 NENO
Umati mkubwa, umati mkubwa katika bonde la uamuzi! Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu ni karibu katika bonde la uamuzi. Jua na mwezi vitatiwa giza, na nyota hazitatoa mwanga wake tena. Mwenyezi Mungu atanguruma kutoka Sayuni na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu; dunia na mbingu vitatikisika. Lakini Mwenyezi Mungu atakuwa kimbilio la watu wake, ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli. “Ndipo mtajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Yerusalemu utakuwa mtakatifu; kamwe wageni hawatauvamia tena. “Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa; mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji. Chemchemi itatiririka kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu na kunywesha Bonde la Shitimu. Lakini Misri itakuwa ukiwa, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda, ambao katika nchi yao walimwaga damu isiyo na hatia. Yuda itakaliwa na watu milele na Yerusalemu itadumu vizazi vyote. Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe, nitasamehe.”