Yoeli 3:14-21
Yoeli 3:14-21 SRUV
Umati mkubwa, umati mkubwa, wamo katika bonde la kukata kauli! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata kauli. Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Naye BWANA atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka; lakini BWANA atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli. Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe. Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya BWANA, na kulinywesha bonde la Shitimu. Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao. Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi. Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana BWANA ndiye akaaye Sayuni.