Yoeli 3:14-21
Yoeli 3:14-21 BHN
Wanafika makundi kwa makundi kwenye bonde la Hukumu, maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia. Jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu ananguruma huko Siyoni; sauti yake inavuma kutoka Yerusalemu; mbingu na dunia vinatetemeka. Lakini Mwenyezi-Mungu ni kimbilio la watu wake, ni ngome ya usalama kwa Waisraeli. “Hapo, ewe Israeli, utajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nakaa Siyoni, mlima wangu mtakatifu, Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu; na wageni hawatapita tena humo. “Wakati huo, milima itatiririka divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa. Vijito vyote vya Yuda vitajaa maji; chemchemi itatokea nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, na kulinywesha bonde la Shitimu. “Misri itakuwa mahame, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu waliwashambulia watu wa Yuda wakawaua watu wasio na hatia. Bali Yuda itakaliwa milele, na Yerusalemu kizazi hata kizazi. Nitawaadhibu waliomwaga damu ya watu wa Yuda wala sitawaachia wenye hatia. Mimi, Mwenyezi-Mungu nakaa Siyoni.”