Mathayo 15:29-39
Mathayo 15:29-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto. Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani.
Mathayo 15:29-39 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli. Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.
Mathayo 15:29-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena sitaki kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto. Akawaaga makutano, akapanda katika mashua, akaenda pande za Magadani.
Mathayo 15:29-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli. Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.” Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.