Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 18:5-14

Mathayo 18:5-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari. “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya yale mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha. Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa jehanamu. “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [ Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.] “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

Shirikisha
Soma Mathayo 18