Mathayo 27:27-44
Mathayo 27:27-44 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Wakaketi, wakawa wanamchunga. Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
Mathayo 27:27-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo askari wa mtawala wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji la miiba, wakaliweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kulia; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampigapiga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulubisha. Walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la Kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulubisha, waligawana mavazi yake, kwa kupiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko. Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulubiwa pamoja naye, mmoja katika mkono wake wa kulia, na mmoja katika mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang'anyi waliosulubiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
Mathayo 27:27-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha. Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko. Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang’anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
Mathayo 27:27-44 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha wakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe. Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. Walipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] Kisha wakaketi, wakamchunga. Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini. Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.