Mathayo 27:45-56
Mathayo 27:45-56 Biblia Habari Njema (BHN)
Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.” Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.” Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
Mathayo 27:45-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hadi saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliokuweko, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule afisa, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la ardhi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Mathayo 27:45-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Mathayo 27:45-56 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.” Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake. Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi. Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.