Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 12:28-37

Marko 12:28-37 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Isa amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?” Isa akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwalimu wa Torati akamwambia Isa, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. Kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, na kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.” Isa alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe huko mbali na ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena. Isa alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa Torati wanasema kwamba Al-Masihi ni Mwana wa Daudi? Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, alisema: “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.”’ Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?” Umati ule wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.

Shirikisha
Soma Marko 12