Marko 2:18-28
Marko 2:18-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kufunga wakati bwana arusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana arusi hawawezi kufunga. Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. “Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama wakifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!” Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukata masuke ya ngano. Mafarisayo wakawaambia, “Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake.” Basi, Yesu akawaambia, “Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato! Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ana uwezo hata juu ya Sabato.”
Marko 2:18-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; akishona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya. Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa akiona njaa na kuhitaji chakula, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.
Marko 2:18-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya. Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.
Marko 2:18-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga. Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga. “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi. Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.” Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula? Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.” Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”