Marko 2:18-28
Marko 2:18-28 SRUV
Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; akishona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya. Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa akiona njaa na kuhitaji chakula, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.