Marko 2:18-28
Marko 2:18-28 NEN
Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga. Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga. “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi. Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.” Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula? Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.” Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”