Methali 13:1-25
Methali 13:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtoto mwenye hekima husikia maagizo ya baba yake, lakini mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu mwema hupata mema kutokana na maneno yake, lakini wadanganyifu huishi kwa ukatili. Achungaye mdomo wake huyahifadhi maisha yake, anayeropoka ovyo hujiletea maangamizi. Mvivu hutamani lakini hapati chochote, hali mwenye bidii hujaliwa riziki kwa wingi. Mwadilifu huuchukia uongo, lakini mwovu hutenda kwa aibu na fedheha. Uadilifu huwalinda wenye mwenendo mnyofu, lakini dhambi huwaangusha waovu. Baadhi hujidai kuwa matajiri kumbe hawana kitu; wengine hujiona kuwa maskini hali wana mali tele. Fidia ya mtu ni mali yake, lakini maskini hana cha kutishwa. Mwadilifu hungaa kama taa iwakayo vizuri, lakini waovu ni kama taa inayozimika. Kiburi husababisha tu ugomvi, lakini kwa wanaokubali shauri jema mna hekima. Mali ya harakaharaka hutoweka, lakini akusanyaye kidogokidogo ataiongeza. Tumaini la kungojangoja huumiza moyo, lakini tazamio linalotimia ni mti wa uhai. Anayedharau mawaidha anajiletea maangamizi, lakini anayetii amri atapewa tuzo. Mafundisho ya wenye hekima ni chemchemi ya uhai; humwezesha mtu kuiepa mitego ya kifo. Kuwa na akili huleta fadhili, lakini njia ya waovu ni ya taabu Mwenye busara hutenda kila kitu kwa akili, lakini mpumbavu hutembeza upumbavu wake. Mjumbe mbaya huwatumbukiza watu taabuni, lakini mjumbe mwaminifu huleta nafuu. Umaskini na fedheha humpata asiyejali mafundisho, lakini mwenye kusikia maonyo huheshimiwa. Inafurahisha upatapo kile unachotaka, kwa hiyo wapumbavu huchukia kuepa uovu. Anayeandamana na wenye hekima hupata hekima, lakini anayejiunga na wapumbavu atapata madhara. Watendao dhambi huandamwa na balaa, lakini waadilifu watatuzwa mema. Mtu mwema huwaachia urithi uzao wake, lakini mali ya mwenye dhambi imerundikiwa waadilifu. Shamba la maskini hutoa mazao mengi, lakini bila haki hunyakuliwa. Asiyemwadhibu mtoto wake hampendi; lakini ampendaye mwanawe humrudi mapema. Mwadilifu anacho chakula cha kumtosheleza, lakini tumbo la waovu hutaabika kwa njaa.
Methali 13:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu; Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote. Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika. Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. Kila anayelidharau neno hujiletea uharibifu; Bali yeye anayeiogopa amri atapewa thawabu. Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya muasi huangamiza. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. Nenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. Uovu huwafuatia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma. Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.
Methali 13:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote. Nuru ya mwenye haki yang’aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika. Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu. Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma. Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.
Methali 13:1-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri. Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia. Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu. Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha. Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi. Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi. Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho. Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana, bali taa ya mwovu itazimwa. Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri. Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka. Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima. Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo. Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti. Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu. Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake. Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji. Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa. Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya. Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima, bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara. Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki. Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali. Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha. Mwenye haki hula mpaka akaridhisha moyo wake, bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.