Methali 8:1-36
Methali 8:1-36 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni! Hekima anaita! Busara anapaza sauti yake! Juu penye mwinuko karibu na njia, katika njia panda ndipo alipojiweka. Karibu na malango ya kuingilia mjini, mahali wanapoingia watu anaita kwa sauti: “Enyi watu wote, nawaita nyinyi! Wito wangu ni kwa ajili ya binadamu. Enyi wajinga, jifunzeni kuwa na akili; sikilizeni kwa makini enyi wapumbavu. Sikilizeni maana nitakachosema ni jambo muhimu; midomoni mwangu mtatoka mambo ya adili. Kinywa changu kitatamka kweli tupu; uovu ni chukizo midomoni mwangu. Kinywa changu kitatamka maneno ya kweli, udanganyifu ni haramu midomoni mwangu. Kwa mtu mwelewa kila kitu ni wazi, kwa mwenye maarifa yote ni sawa. Chagua mafundisho yangu badala ya fedha; na maarifa badala ya dhahabu safi. “Mimi Hekima nina thamani kuliko johari; chochote unachotamani hakiwezi kulingana nami. Mimi Hekima ninao ujuzi; ninayo maarifa na busara. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni kuchukia uovu. Nachukia kiburi, majivuno na maisha mabaya; nachukia na lugha mbaya. Nina uwezo wa kushauri na nina hekima. Ninao ujuzi na nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme hutawala, watawala huamua yaliyo ya haki. Kwa msaada wangu viongozi hutawala, wakuu na watawala halali. Nawapenda wale wanaonipenda; wanaonitafuta kwa bidii hunipata. Utajiri na heshima viko kwangu, mali ya kudumu na fanaka. Matunda yangu ni mazuri kuliko dhahabu safi, faida yangu yashinda ile ya fedha bora. Natembea katika njia ya uadilifu; ninafuata njia za haki. Mimi huwatajirisha wanaonipenda, huzijaza tele hazina zao wanipendao. “Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote. Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari; wakati alipoimarisha mawingu mbinguni, alipozifanya imara chemchemi za bahari; wakati alipoiwekea bahari mpaka wake, maji yake yasije yakavunja amri yake; wakati alipoiweka misingi ya dunia. Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi, nilikuwa furaha yake kila siku, nikishangilia mbele yake daima, nikifurahia dunia na wakazi wake, na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu. “Sasa basi wanangu, nisikilizeni: Heri wale wanaofuata njia zangu. Sikilizeni mafunzo mpate hekima, wala msiyakatae. Heri mtu anayenisikiliza, anayekaa kila siku mlangoni pangu, anayekesha karibu na milango yangu. Anayenipata mimi amepata uhai, amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu. Asiyenipata anajidhuru mwenyewe; wote wanaonichukia wanapenda kifo.”
Methali 8:1-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake? Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo. Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele. Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu. Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu. Sikilizeni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili. Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi. Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa. Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo. Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa makao yangu; Natafuta maarifa na busara. Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia. Ushauri ni wangu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia. Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu ni bora kuliko dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu ni bora kuliko fedha iliyo safi. Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao. BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nilitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijakuwako dunia. Wakati havijakuwapo vilindi nilizaliwa, Wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nilizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala mashamba Wala chanzo cha udongo wa dunia; Alipozithibitisha mbingu nilikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.
Methali 8:1-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake? Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo. Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele. Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu. Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu. Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili. Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi. Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa. Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo. Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; Natafuta maarifa na busara. Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia. Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia. Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule. Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao. BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.
Methali 8:1-36 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Je, hekima haitani? Je, ufahamu hapazi sauti? Juu ya miinuko karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo; kando ya malango yaelekeayo mjini, kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema: “Ni ninyi watu, ninaowaita; ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote. Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili; ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu. Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema; ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa. Kinywa changu husema lililo kweli, kwa maana midomo yangu huchukia uovu. Maneno yote ya kinywa changu ni ya haki; hakuna mojawapo lililopotoka au la ukaidi. Kwa wenye kupambanua, yote ni sahihi; hayana kasoro kwa wale wenye maarifa. Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi, kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye. “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara; ninamiliki maarifa na busara. Kumcha Mwenyezi Mungu ni kuchukia uovu; ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu. Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu; nina ufahamu na nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme hutawala na watawala hutunga sheria zilizo za haki, kwa msaada wangu wakuu hutawala, na wenye vyeo wote watawalao dunia. Nawapenda wale wanaonipenda, na wale wanaonitafuta kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri unaodumu na mafanikio. Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile ninachotoa hupita fedha iliyo bora. Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki, nawapa utajiri wale wanaonipenda na kuzijaza hazina zao. “Mwenyezi Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani; niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa. Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji; kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa, kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia. Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho kwenye uso wa kilindi, wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari, wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia. Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake, nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu. “Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu. Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze. Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu. Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima, na kujipatia kibali kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanaonichukia mimi hupenda mauti.”