Mithali 8
8
Wito wa hekima
1Je, hekima haitani?
Je, ufahamu hapazi sauti?
2Juu ya miinuko karibu na njia,
penye njia panda, ndipo asimamapo;
3kando ya malango yaelekeayo mjini,
kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
4“Ni ninyi watu, ninaowaita;
ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
5Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili;
ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
6Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema;
ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
7Kinywa changu husema lililo kweli,
kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
8Maneno yote ya kinywa changu ni ya haki;
hakuna mojawapo lililopotoka au la ukaidi.
9Kwa wenye kupambanua, yote ni sahihi;
hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
10Chagua mafundisho yangu badala ya fedha,
maarifa badala ya dhahabu safi,
11kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani
na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye.
12“Mimi hekima, nakaa pamoja na busara;
ninamiliki maarifa na busara.
13Kumcha Mwenyezi Mungu ni kuchukia uovu;
ninachukia kiburi na majivuno,
tabia mbaya na mazungumzo potovu.
14Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu;
nina ufahamu na nina nguvu.
15Kwa msaada wangu wafalme hutawala
na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
16kwa msaada wangu wakuu hutawala,
na wenye vyeo wote watawalao dunia.
17Nawapenda wale wanaonipenda,
na wale wanaonitafuta kwa bidii wataniona.
18Utajiri na heshima viko kwangu,
utajiri unaodumu na mafanikio.
19Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi;
kile ninachotoa hupita fedha iliyo bora.
20Natembea katika njia ya unyofu
katika mapito ya haki,
21nawapa utajiri wale wanaonipenda
na kuzijaza hazina zao.
22“Mwenyezi Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake,
kabla ya matendo yake ya zamani;
23niliteuliwa tangu milele,
tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
24Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa,
wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji;
25kabla milima haijawekwa mahali pake,
kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa,
26kabla hajaumba dunia wala mashamba yake
au vumbi lolote la dunia.
27Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake,
wakati alichora mstari wa upeo wa macho
kwenye uso wa kilindi,
28wakati aliweka mawingu juu
na kuziweka imara chemchemi za bahari,
29wakati aliiwekea bahari mpaka wake
ili maji yasivunje agizo lake,
na wakati aliweka misingi ya dunia.
30Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake.
Nilijazwa na furaha siku baada ya siku,
nikifurahi daima mbele zake,
31nikifurahi katika dunia yake yote
nami nikiwafurahia wanadamu.
32“Basi sasa wanangu, nisikilizeni;
heri wale wanaozishika njia zangu.
33Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;
msiyapuuze.
34Heri mtu yule anisikilizaye mimi,
akisubiri siku zote malangoni mwangu,
akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
35Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima,
na kujipatia kibali kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
36Lakini yeyote ashindwaye kunipata
hujiumiza mwenyewe;
na wote wanaonichukia mimi hupenda mauti.”
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.